Monday, June 24, 2013

CHADEMA yafichua njama nzito kuiua


MBOWE, SLAA, LISSU, MNYIKA WAANDALIWA KESI YA TINDIKALI IGUNGA
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuna mpango mchafu wa kuwabambikizia viongozi wakuu wa chama hicho kesi ya kumwagiwa Tindikali kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Musa Tesha.
Viongozi wanaoandaliwa mpango huo ni Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, Mnyika alisema mpango huo unafanyika kwa lengo la kukidhoofisha chama chao kinachowapa wakati mgumu CCM.
Alisema hivi sasa baadhi ya makachero wa polisi wamekuwa wakiwakamata vijana na kuwalazimisha kukiri kwa kuandika au kuandikiwa maelezo kuwa viongozi hao waliwatuma kummwagia tindikali Tesha wakati wa uchaguzi mdogo wa Igunga mwaka 2011.
Mnyika alisema wafuasi wao waliokamatwa na polisi kwa kuhusishwa na tukio hilo wameshinikizwa kusema Mbowe, Slaa, Lissu na yeye ndio waliowatuma kummwagia tindikali Tesha.
Alisema jambo hilo linaendeshwa kisiasa, ambapo wafuasi wanne wameshatiwa mbaroni na kuwalazimisha kuwataja viongozi wakuu wa CHADEMA kuhusika na uhalifu huo.
Mnyika aliwataja waliokamatwa ni pamoja na Evodius Justinian, aliyeshikiliwa kwa siku mbili mjini Bukoba, na baadaye akapelekwa Mwanza kabla ya kufikishwa Dar es Salaam.
Alisema zoezi hilo lilifanyika kwa kificho na mtuhumiwa huyo baadae alifikishwa Igunga.
Alibainisha kuwa taarifa za kada huyo kupelekwa Dar es Salaam  zilikuwa za kificho kwani wakili wake, Nyaronyo Kicheere aliyeongozana na ndugu wa mtuhumiwa huyo walipofika Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam walielezwa amepelekwa Makao Makuu.
Mnyika alisema mara baada ya Evodius kuonana na wakili wake, Kicheere, siku hiyo alieleza unyama aliofanyiwa na jeshi hilo wakati wote wa mahojiano mkoani Mwanza na Dar es Salaam.
Katika maelezo yake yaliyoshuhudiwa na Ofisa wa Polisi Makao Makuu, Advocate Nyombi, Evodius alisema kuwa baada ya kutolewa mjini Bukoba kwa siri bila ndugu zake kujua, alipelekwa jijini Mwanza na kuhojiwa bila kuruhusiwa kuonana na wakili wake.
Kada huyo akisimulia unyama aliofanyiwa alisema:  “Nimepigwa na polisi Mwanza, nikiwa chooni Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam wakati naletwa huku, polisi wakaniambia mimi ni mtu hatari sana, niseme nilifanya nini Igunga na kama najua mkanda wa Lwakatare.
“Nikiwa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam niliomba kwenda chooni, waliingia pamoja na mimi wakanipiga sana, nimeshaandika maelezo kwa kulazimishwa, niliomba kuwa na wakili wakanikatalia.”
Aliongeza kuwa akiwa Dar es Salaam alihojiwa aseme ukweli kuhusu video ya Lwakatare. Akawajibu kuwa ilifanyiwa uhariri na Ludovick, lakini akapigwa makofi na askari wakaagiza nyaya za umeme za kutesea.
“Waliposimama kuleta nyaya za umeme, kwa kuhofia mateso ya umeme nikasema hii video ni yangu. Ninaumwa sana tumbo la kuhara damu, natumia dawa nilizonunuliwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Kagera tarehe 4 Aprili,” alisema.
Mnyika alisema mtuhumiwa wa pili aliyeteswa ili akubali kuandika kuwa Mbowe, Slaa, Lissu na Mnyika walimtuma akammwagie tindikali Tesha ni Seif Kabuta aliyekamatwa Mwanza.
Alisema Kabuta baada ya kukataa kukiri kuwa viongozi wake wanahusika na matendo hayo, walimfungia katika chumba maalumu wakamleta mke wake, mama yake na mkwe wake na kumtesa mbele yao ili akiri kuwa Mbowe na wenzake walimtuma kummwagia Tesha tindikali.

No comments:

Post a Comment