TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.

Itakumbukwa tarehe 02/09/2012 katika operesheni za Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) mkoani Iringa kulitokea vurugu zilizosababisha kuuawa kwa mwanahabari mzoefu Ndg. Daudi Mwangosi na kujeruhiwa vibaya kwa *askari watatu wa kuzuia fujo.

Chama Cha Mapinduzi kimepokea kwa masikitiko makubwa sana taarifa za kifo hicho na kujeruhiwa kwa askari hao. CCM inachukua nafasi hii kutoa pole kwa wafiwa, wanahabari nchini na wote walioguswa na msiba huu kwa namna moja au nyingine.*

Tunatoa wito kwa vyombo na tume mbalimbali zilizoundwa kuchunguza swala hili, vichunguze kwa umakini na weledi mkubwa ili kubaini yote - ikiwemo chanzo cha vurugu zilizotokea na mazingira ya kifo cha ndugu yetu Daudi Mwangosi.*

Pamoja na wito wetu wa kuchunguzwa suala hili kwa umakini na weledi mkubwa, pia tunatoa rai kwamba uchunguzi huu ufanyike kwa kutumia muda mfupi ili ukweli uweze kubainika mapema na hatua zinazostahili ziweze kuchukuliwa haraka iwezekanavyo.

Vilevile CCM inasikitishwa sana na mfululizo wa matukio ya watu kupoteza maisha au kujeruhiwa katika mikutano na operesheni mbalimbali zinazoendeshwa na CHADEMA nchini hasa zile zilizofanyika kwa kukaidi amri halali za vyombo vya ulinzi na usalama. *

Kutaja matukio baadhi tu ni pamoja na lile la kuuwawa kwa kada wa CCM Mkoani Singida, kuuawa kwa Ndg. Ally Hassan mjini Morogoro, kuuawa kwa Ndg. Daudi Mwangosi Mjini Iringa hivi majuzi,kujeruhiwa kwa askari polisi Iringa na matukio mengine mengi ambayo yametokea wakati wenzetu wa CHADEMA wakiendesha operesheni zao mbalimbali nchini.

Matukio haya si mazuri kutokea kwenye shughuli za Chama cha siasa. Kwakweli ni aibu, inayohitaji uwajibikaji,hata kama ni wa kisiasa. Inapotokea shughuli za chama chako zinasababisha kupotea kwa maisha ya watu kila unapozifanya na bado usitake kuwajibika, inahitaji roho ngumu na ujasiri wa aina yake.

Inakuwa mbaya zaidi pale vifo hivi vinaposababishwa na Chama hicho kutotii amri halali zilizotolewa kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi inayovipa pia uhalali *vyama vya siasa kuwepo na kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria.*

Laiti Chama hicho kingesubiri siku chache zilizobakia kabla ya Sensa kuisha kabla ya kuendelea na mikutano yake ni dhahiri mauaji haya yasingetokea. Lakini kauli za kukebehi na uamuzi wa kukaidi amri ya Jeshi la Polisi na kusema "tupo tayari kwa lolote" ni ishara kwamba Chama hiki kiliandaa na kujiandaa na fujo zilizotokea.

Tunatoa wito kwa vyama vya siasa na wanasiasa kwa ujumla kujenga utamaduni wa kuheshimu utawala wa sheria. Amani na utulivu vulivyopo nchini ni kazi nzuri iliyojengwa kwa muda mrefu na waasisi wetu kwa kujenga utamaduni wa kuzingatia utawala wa sheria.

Imetolewa na;
Nape Moses Nnauye
Chama Cha Mapinduzi
Katibu wa NEC-Itikadi na Uenezi Taifa.