Friday, September 21, 2012

KUMBE LILILOKO BUNGENI HALIRUHUSIWI KUJADILIWA NJE YA HAPO?




Veronica Kazimoto, MAELEZO

Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imetoa tamko la kuwataka watendaji wa Serikali, Mahakama, vyombo vya habari na taasisi nyingine zote kuacha kuzungumzia suala la Uteuzi wa Majaji wa mahakama kuu kama lilivyowasilishwa Bungeni wakati wa Mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2012/13.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Brigedia Jenerali Mstaafu Hassan Ngwilizi (Mb), amesema suala hilo liko mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo inaendelea na uchunguzi hivyo haitarajiwi taasisi nyingine, nje ya Bunge kulizungumzia suala hili kwa kuwa linajadiliwa.

“Kamati imeamua kutoa tamko hili kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa uvunjifu wa kanuni na taratibu tulizojiwekea kwa mujibu wa Katiba na Sheria nyingine za nchi kutoendelea kuvunjwa,” amesema Ngwilizi.

Ngwilizi amenukuu Ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayosema kuwa kutakuwa na Uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu Katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, au katika mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge.

“Uhuru wa utaratibu unaohifadhiwa na ibara hiyo ya Katiba umelipa Bunge mamlaka ya kujiwekea utaratibu wa kushughulikia masuala yake katika Kanuni za Kudumu za Bunge zilizotungwa chini ya Ibara ya 89 (1) ya Katiba”, amesisitiza Ngwilizi.

Kutolewa kwa tamko hilo na kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kunatokana na mwongozo ulioombwa na Gosbert Blandes (Mb) wakati wa Hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara ya Katiba na Sheria,Tundu Lissu Mbunge wa Singida Mashariki.

Katika maelezo yake, Blandes alinukuu ukurasa wa 9 aya ya 2 katika hotuba hiyo iliyosomeka kuwa watu wanateuliwa kuwa majaji wa mahakama Kuu ambao hawajawahi kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Aya hiyo iliendelea kusema kuwa inaelekea watu hao hupewa ujaji kama zawadi ili kuwawezesha kupata mafao ya majaji wastaafu ambayo yameboreshwa na matokeo yake ni kuwa na majaji ambao wamechoka na hawawezi au hawajui namna ya kufanya kazi ya jaji wa mahakama kuu.

No comments:

Post a Comment