Wednesday, September 26, 2012

ASKARI AJINYONGA

ASKARI polisi mwenye cheo cha koplo, Mlima Mnyasi ‘Katafunua’ wa Kituo cha Kilwa Road Mkoa wa Kipolisi wa Temeke jijini Dar, hivi karibuni alikutwa amejinyonga hadi kufa katika lori la polisi lililopo kituoni hapo.

Mnyasi mwenye namba C.8909 alikutwa na askari mwenzake Septemba 16, mwaka huu, majira ya asubuhi akiwa amejinyonga kwa kutumia kamba za viatu huku chanzo cha kifo chake kikidaiwa ni kukaa kazini muda mrefu bila ya kupandishwa cheo.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari ndani ya jeshi hilo, Koplo Mnyasi kabla ya kifo chake alikuwa akinung’unika mara kwa mara juu ya suala hilo huku akishuhudia wenzake alioanza nao kazi wakipandishwa vyeo.

“Kila mtu anasema lake lakini mimi nakwambia huyu amejinyonga baada ya kuona wenzake wanapandishwa vyeo, yeye yuko pale pale. Hivi karibuni baadhi ya polisi walipelekwa katika vyuo mbalimbali vya polisi kikiwemo kile kilichopo Zanzibar. Koplo Mnyasi naye alichukua begi lake akiamini jina lake limo katika orodha ya askari waliopendekezwa. Alipofika kule, akaambiwa jina lake halimo. Alishangaa sana na ndipo alipochukua begi lake na kurejea kwenye kituo chake cha kazi.Haikuchukua muda mrefu ndipo umauti ukamkuta katika mazingira hayo na ndiyo maana wengi wanaamini kucheleweshewa cheo ndiyo sababu,” kilidai chanzo hicho.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, David Misime alipoulizwa kuhusiana na kifo hicho alikiri kuwepo kwa askari huyo kujinyonga lakini chanzo cha kifo chake bado hakijajulikana.

No comments:

Post a Comment