Siku za karibuni Watanzania tulipopo katika tovuti jamii tumeshuhudia
kitu ambacho nakiita “Series”. Kwa bahati mbaya imenichukua muda
kuishtukia series yenyewe kwa hiyo ni ngumu sana kusema tuko season ya
ngapi na episode gani.
Picha lenyewe lilianzia Jamii Forums
ambako kambi za wanasiasa wambao wanaoneakana wamejiandaa kuichukua
nchi katika uchaguzi mkuu 2015 zilianza kujionyesha wazi wazi moja ikiwa
ni ya waziri mkuu alietema mzigo awamu ya kwanza Edward Lowassa na
nyingine ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Edward
Membe. Kwa upande wa JF
hizi kambi hazijifichi, tunawajua kina nani ni mashabiki wa nani na
kina nani wanampinga nani. JF sina tatizo kwa sababu kusema kweli kule
ndio Social Network ambayo kila kichwa ambacho kinajua siasa kipo na
ndio maana ikaitwa The Home Of Great Thinkers.
Kitu kinachonikera ni kitendo cha hawa wataka madaraka kuvamia sehemu
ambazo Watanzatulikuwa tumekaa kwa amani bila kuleteana stress na
kuchoshana, Faceboook na Twitter. Na style waliyoingia nayo ni ile ya
kuchafuana. Tulianza na Mkurugenzi wa Habari Ikulu ndugu Salva Rweyemamu, account yake ikawa hacked na mtu asiejulikana wakati huo Rais Kikwete
alikuwa anajiandaa kwenda kwenye safari yake ya Australia. Aliehack
akaanza kuweka madude ya ajabu na akafollow watu kibao twitter, kila mtu
alijua kabisa kuwa Salva kawa hacked kwa hiyo hakuna aliejali sana.
Kinachonishangaza ni kitendo cha Salva Rweyemamu mwenyewe kutokanusha
kwenye vyombo vya habari kama vya serikali ambayo yeye ndo kama msemaji
na pia mpika propaganda zote zinazotoka mle ndani ya Ikulu kwenda
Magazeti yanayomilikiwa na serikali. Ameacha tu jamaa anaendelea kupeta.
Haya, Wakati picha la Salva linaanza kupoteza mvuto mara kaibuka Mama.. aliingia mama First Lady
kupitia account yake ambayo ilikuwa inatumika toka wakati wakati wa
Kampeni za uchaguzi 2010 mara ghafla bin vuu tukaona anaanza
“kum-snitch” mumewe tena ikiwa ni ile wiki ya Mheshimiwa Kikwete
kukutana na CHADEMA
ikulu kuhusu majadiliano ya sheria mpya ya uundwaji wa Katiba. Sihitaji
kusimulia kilichotokea kwenye account ya Bi Mkubwa unaweza kusoma
Timeline yake kwa kubofya hapa.
Mara wakati tunaanza kupiga miluzi na kuanza kuona Mama hana jipya,
siku ya Jumanne Desemba 6 parapanda likalia, mtu tulieamini kwamba kwa
sasa yuko kwenye bohari la kusubiria siku ya hukumu ili tujue kama
unaenda Ahera au Kuzimu sio mwingine bali Gavana wa Benki Kuu ambaye
alitupiwa kila zigo la misumari ya madudu yaliyofanyika kwenye kashfa
za ufujaji wa hela za wananchi katika Benki Kuu Tanzania “BOT” ndugu
Daudi Balali nae akaibuka twitter na jina lake lile lile la Daudi Balali.
Huyu jamaa nimekuja kushtukia kuwa ananifollow kama saa moja jioni na
kabla ya hapo niliangalia followers wangu wapya saa sita alasiri
ikimaanisha ndani ya hayo masaa matano baada ya mimi kuangalia jamaa
alifungua account akaanza kufollow watu na kwa namna twitter kule
mbinguni/motoni ilivyo fasta ndani ya hayo masaa machache kafollow
watanzania kibao. Anachodai jamaa mwenyewe anasema yeye hajafa na yuko
visiwa flani anakula raha na kashasema kuwa ana siri za kutuambia kuhusu
kifo chake ambazo kiujumla lazima ziwataje Wanasiasa wa Tanzania.
Kitu tunachotakiwa kujiuliza ni je kwa nini hawa watu wanaofanya huu
upuuzi wa kuibiana password wanaonekana kuwa na kasi ya ajabu na hakuna
mtu au kiongozi yeyote serikalini au wizara husika anaeonekana kujali
kuhusu hili suala la majina ya Watu walioko ndani ya Utawala wa Rais
Kikwete kutumiwa vibaya kwenye mitandao ya kijamii? Tuliona Wizara ya
Mambo ya ndani ilivyoshadadia ule waraka uliowekwa Jamii Forum na baadae
kusambazwa kwenye email kwa watu mbalimbali kuhusu Kikosi kilichotoa
onyo kuwa kinataka kumpindua Rais Kikwete. Mheshimiwa Shamsi Vuai
Nahodha waziri wa Mambo ya Ndani alitupiga mikwara kuwa yeyote
atakae-forward hiyo email atachukuliwa hatua za kisheria na tukaogopa
ule waraka umekufa bila kelele. Sasa ni kwa nini hatua hiyo hiyo
haijachukuliwa kwa mtu anaeendeleza huo mchezo twitter na facebook
ameachiwa aweke kitu anachokitaka?
Kinachoonekana hapa ni kuwa hawa wanasiasa sasa wameamua kutuvamia
kwenye social media, staili waliyoingia nayo ndio bado sijajua ni kambi
ya nani inahusika. Wamegundua kwamba sasa hivi watu tunapenda kujadili
mambo yanayotokea kwenye ulingo wa siasa kwa kuongea ukweli bila
kumuogopa mtu na tumekuwa tukiikosoa wazi wazi serikali pale inapokosea.
Na bila kujijua tumeukwaa mtego wao, wanapoanza kuongea mambo yao
tunawashabikia mimi nikiwa mmoja wapo ambao nilimshangilia bi mkubwa
alipoanza kumnanga wazi mumewe. Kitu tunachotakiwa kujua ni kuwa hawa
watu wamekuja na mkakati mpya, wanajua wazi kuwa wanao uwezo mkubwa wa
kutawala vyombo vya Habari vya ndani kama Magazeti na Redio. Tunaona
wenyewe namna magazeti siku hizi yalivyojaa ushabiki wa vyama. Kuonyesha
namna walivyopania kutukukamata wamepiga hatua kubwa zaidi kwa kununua
baadhi ya wamiliki wa blog, hili najua kila mtu analifaham. Kuna
bloggers ambao miaka michache iliyopita walikuwa mstari wa mbele kutetea
haki za Wananchi lakini sasa hivi hatunao ghafla wamekuwa mazezeta na
wanasema hewala kwa kila kitu kinachotokea serikalini ingawa mwisho wa
siku wanaaibika. Kitu kilichowashinda mpaka sasa ni namna ya kuwanunua
watu kama Udadisi, Chahali, Maria Sarungi, Michael Dalali, Yericko Nyerere, Issa Mwamba, Mshaba, Irenei, Semkae, iAlen,tsavonglah, omarilyas, Nanyaro Patrick
na wengine wengi sijawataja ambao wamekuwa na fikra zisizoyumbishwa na
matukio yao wanayoyatengeneza ili kutuvuruga. Wanajua hawawezi kuweka
ofa mezani ya kutunyamanzisha wote kwa pamoja, wanajua hizi website ni
za mzungu na hawana uwezo wa kutuchagulia tuongee nini na kwa wakati
gani kwa hiyo wameamua kutuundia mkakati wa kuhakikisha kinatokea kile
ambacho wazungu wanaita “divide and rule”.
Tunatakiwa kujua kitu kimoja, hawa watu wanaofanya huu mchezo wapo
kati yetu, ni marafiki zetu ambao inawezekana hata tunapokuwa tunajadili
siasa na wao ni wachangiaji wazuri tu ila wanajifanya anti-government.
Tatizo ni kwamba hatuwafahamu kwa majina, wanarusha ngumi gizani alaf
wanasikilizia nani atatoa mguno wa maumivu. Kama kweli tunataka uwepo
wetu mtandaoni usionekane kuwa ni wa kihuni tujitahidi sana kuwapotezea
hawa watu. Unapozidi kumsemesha mtu kama balali inamaanisha sio kwamba
wewe tu ndio utakuwa unajibizana nae, kumbuka kuna followers wako ambao
wanakuwa wanafatilia mnachoongea na kuweka RT kwa hiyo inasambaa kwa
familia ya Watanzania wote mtandaoni. Kama kweli tunataka kukomesha hii
tabia ya kutufanya mabwege na mazezeta kwa kutuchagulia habari gani
tuisikie tunatakiwa tuwapotezee, wakiongea kaa kimya wala usipoteze muda
kuongea nao. Usitegemee kuwa huyo anaejiita balali au mama salma
atakuja na jipya zaidi ya propaganda ambazo mwisho wa siku ni za
kumfanya mtu fulani apate kura 2015. Njia wanayoitumia hapa ni kuongea
kitu ambacho wanajua Watanzania wengi wanakijadili kila siku, serikali.
Wamekuwa mstari wa mbele kuikosoa serikali. Kabla hujashabikia tambua
kwamba hawa sio wenzetu. Wakati wewe unaikosoa serikali kwa kufikiria
vizazi vijavyo wao wamelenga kura yako na uchaguzi mkuu ujao 2015.
Tambua kitu kimoja, Wapo kati yetu. Daktari Jakaya aliseka “Za kuambiwa Changanya na Zako”
Ni Hayo tu.
No comments:
Post a Comment