Monday, December 19, 2011

Chelsea yapoteza pointi

Jordi Gomez alisawazisha baada ya dakika 87 na kupunguza kasi ya Chelsea katika juhudi za kufikia kilele cha ligi kuu ya Premier, na kuiwezesha timu yake ya Wigan kupata pointi muhimu katika kujinusuru kusalia katika ligi kuu.
Katika kipindi cha kwanza, Wigan walihisi walistahili kupata nafasi ya kupiga mkwaju wa penalti, baada ya mpira kutoka kwa Victor Moses kuugusa mkono wa Branislav Ivanovic.
Chelsea waliimarisha mchezo wao, na katika kipindi cha pili, Daniel Sturridge alitia mpira wavuni baada ya kupigiwa mpira na Ashley Cole.
Lakini Wigan hawakuogopa jina kubwa la Chelsea, na kufuatia mpira kumponyoka kipa Petr Cech, Gomez alitumbukiza mpira wavuni, na mechi kumalizika kwa sare ya 1-1.
Katika viwanja vingine, mechi za awali, Blackburn walishindwa magoli 2-1 walipocheza na West Brom.
Everton ilitoka sare ya 1-1 ilipokutana na Norwich.
Fulham ilithibitisha ngome ya Bolton bado ni dhaifu kwa kuwafunga magoli 2-0 kwa kirahisi.
Stoke iliishinda Wolves 2-1.
Mechi moja tu ndio ilikosa mabao, wakati Newcastle ilipocheza na Swansea, na wote kuondoka uwanjani 0-0.
Katika mechi za Jumapili, QPR itacheza na Man Utd, Aston Villa dhidi ya Liverpool, Tottenham iko uwanjani kupambana na Sunderland, na katika mechi inayotazamiwa kusisimua sana, Man City ikiongoza ligi itaikaribisha Arsenal.


No comments:

Post a Comment