Barcelona wameshinda kombe la dunia la Fifa kwa vilabu baada ya
kuicharaza timu ya Santos ya Brazil kwa mabao 4-0 kwenye mchezo wa
fainali uliyochezwa nchini Japan.
Ushindi huo umeendeleza rekodi nzuri ya klabu hiyo kwa mwaka huu
ambapo wao ni mabingwa wa Ligi ya Hispania maarufu La Liga, wanashikilia
ubingwa wa vilabu vya Ulaya na pia Kombe la Hispania maarufu Spanish
Super Cup.
Mpachika mabao wa timu ya taifa ya Argentina
Lionel Messi alifunga mabao mawili, huku mengine yakiwekwa kimiani na
Xavi pamoja na nahodha na kiungo wa zamani wa Arsenal Cesc Fabregas.
Ushindi huo unathibitisha kwamba Barcelona inaendelea kusalia timu bora ya kusakata kandanda duniani.
"Tulicheza mchezo wetu kwa ukamilifu," alisema
nahodha Carles Puyol. "Ulikuwa mchezo mzuri, mchezo mgumu sana na
tumefurahi sana kwa matokeo haya."
Mchezo huo baina ya mabingwa wa kandanda wa
Ulaya na wa Amerika Kusini mjini Yokohama ulikuwa ukitajwa kuwa kivutio
kati ya Messi, anayeaminika ndiye mchezaji bora wa soka duniani na
mshambuliaji hatari wa Brazil mwenye umri wa miaka 19 Neymar, ambaye
anatajwatajwa huenda akajiunga na ama na Barca au Real Madrid.
Lakini haikuwa hivyo - Messi akionekana
kushamiri katika mchezo huo na kutajwa mchezaji bora wa mechi hiyo na
pia akapata tuzo ya mchezaji mwenye thamani kubwa katika michuano hiyo
wakati Barcelena ikiweka kibindoni kombe la ubingwa wa dunia kwa mara ya
pili mfululizo katika misimu mitatu.
Bao lake la kwanza alifunga kwa kuubetua mpira
kama ilivyo kawaida yake na la pili alifunga kwa ustadi mkubwa baada ya
kumzunguka mlinda mlango wa Santos Cabral.
Santos walibadilika na kucheza soka nzuri
kipindi cha pili na Neymar nusura afunge baada ya kupatiwa pasi nzuri
akiwa amebakia peke yake na mlinda mlando wa Barcelona Victor Valdes,
lakini Valdes akafanikiwa kuokoa.
"Barcelona walistahili kushinda. Ni timu bora duniani na tumejifunza somo muhimu," alisema Neymar.
Timu ya Qatar ya Al Sadd, ambayo ililazwa mabao
4-0 na Barcelona katika hatua ya nusu fainali, iliwafunga mabingwa wa
Japan Kashiwa Reysol mabao 5-3 kwa mikwaju ya penalti na kufanikiwa
kushika nafasi ya tatu ya michuano hiyo inayofanyika kila mwaka kwa
kushirikisha mabingwa wa soka wa mabara duniani.
No comments:
Post a Comment