Tuesday, July 9, 2013

USHAURI WA MBUNGE KOKA WA KIBAHA

Ben Komba/Pwani-Tanzania/09:46/09/07/2013.
Wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa nchini wameshauriwa kuwa na utamaduni wa kusaidia taasisi mbalimbali za kijamii katika suala zima la kuaharakisha maendeleo ya nchi na wananchi wenyewe.

Hayo yamezungumzwa na mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini, BW.SYLVESTER KOKA wakati akikabidhi msaada wa madawati 50 kwa shule za msingi Jitihada na Lulanzi yaliyotolewa na taasisi ya mikopo kwa wafanyakazi wa umma FAIDIKA.

BW.KOKA amesema kwa jinsi anavyofahamu uwepo wa wafanyabiashara wenye fedha nyingi ambao wangefuata nyayo za Taasisi ya FAIDIKA wangeweza kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Amebainisha kwa sasa nchi yetu ina wafanyabiashara mbalimbali wakubwa ambao kama wangekuwa wanatoa asilimia hata 5 ya walicho nacho katika kuchangia shughuli za kijamii basa kero nyingi za kijamii zingepungua hususan upande wa elimu.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa taasisi ya mikopo ya FAIDIKA, BW.HARUN FERUZ amesema taasisi yake imekuwa na utamaduni wa kuchangia madawati katika maeneo mbali yenye uhitaji ili kuweza kupunguza kero hiyo.

BW. FERUZI ameongeza kuwa kabla ya kutoa madawati hayo, wanafanya utafiti katika shule husika kubaini mahitaji halisi ya madawati na wamekuwa wakitoa kwa kadri ya uwezo wao kutokana na ukosefu wa madawati mashuleni kuwa mgumu.
Akishukuru kwa kupokea madawati hayo Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Lulanzi aliishukuru Taasisi ya mikopo ya FAIDIKA kwa kuweza kutoa mchango huo na kuwataka wafadhili wengine kujitokeza kusaidia shule zenye ukosefu mkubwa wa madawati.

No comments:

Post a Comment