Wednesday, July 24, 2013

MSAJJILI AIONYA CHADEMA

Msajili wa vyama vya Siasa nchini amewaasa wanachama na viongozi wa Chama Cha Democrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutumia muda wao kufanya shughuli za siasa ili kuchangia maendeleo ya nchi badala ya kutumia uwezo na muda wao kubuni mambo yanayoleta mtafaruku na kuhatarisha amani ya nchi.

Pia amepinga tamko la chama hicho la kuanzisha mafunzo ya kujilinda kwa vijana wake nchi nzima.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na kusainiwa kwa niaba ya Msajili wa vyama vya siasa Sisty Nyahoza alisema kuwa hajawahi kuruhusu CHADEMA au chama chochote cha siasa kufanya mafunzo ya ukakamavu au mafunzo ya kutumia nguvu ya aina yoyote kwa wanachama wake au mtu yeyote yule.

Anaongeza kuwa CHADEMA wanaruhusiwa kuanzisha vikundi vya kujilinda lakini hawaruhusiwi kuanzisha mafunzo ya kutumia nguvu kwaajili ya kujilinda kama walivyo tangaza katika mikutano yao ya hadhara kwani ni kinyume na Demokrasia na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano.

Nyahozo ametoa ufafanuzi kuhusu vikundi vya ulinzi na usalama vilivyopo katika Katiba ya Vyama vya Siasa kwamba vikundi hivyo haviruhusiwi kufanya mafunzo ya kutumia nguvu ya aina yoyote katika kutekeleza majukumu yao.

Bali wajibu wao ni kutoa taarifa wa vyombo vya Dola pale wanapo sikia au kuona uhalifu ukitokea na wala sio kupambana na wahalifu au watu wanaotaka kuwadhuru kama tamko la CHADEMA la tarehe 9 mwezi huu linavyo sema.

"Hakuna maelezo yoyote katika Katiba ya CHADEMA yanayoruhusu kutumia nguvu kufanikisha shughuli za kulinda mali na Viongozi wa Chama.Ni vyema wananchi wote waelewe kuwa Sheria za Nchi zimeweka masharti maalumu kwa Vyama Vya Siasa kutokana na umuhimu wa vyama hivi katika kudumisha aman utulivu na umoja wa Kitaifa", alisema Nyahoza.

Alisema kuwa kutokana na Ibara ya20(2)C ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1997 inasema kuwa "Bila kujali masharti ya ibara ya (1) na (4),haitakuwa halali kwa chama chochote cha siasa kuandikishwa ambapo kutokana na katiba au sera yake:-kinakubali au kunapigani matumizi ya nguvu au mapambano kama njia za kufikia malengo yake ya kisiasa.


Nyahoza alimaliza kwa kuwataka CHADEMA kuacha kutekeleza mpango walio tangaza wa kuanzisha makambi ya kufanya mafunzo ya kujilinda kwa vijana wao nchi nzima,kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria za nchi na endapo watashindwa kutii agizo hilo hatua za Kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

No comments:

Post a Comment