"Uchaguzi
mdogo wa Bububu: Mengi yamesemwa toka jana. Naziona hamaki na hasira, nazihisi
hisia za kukata tamaa na kutafishika. Uchaguzi wa Bububu ulikuwa ni zaidi ya
uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi ya Mwakilishi. Haukuwa uchaguzi kati ya CUF na
CCM kama wengi walivyodhania au walivyoutazama. Ulikuwa ni mfano wa kura ya
maoni ndogo kuhusu mwelekeo wa nchi yetu. Ulikuwa ni uchaguzi kati ya wapenda
maridhiano na wayachukiao.
Ulikuwa ni uchaguzi kati ya wapenda maendeleo na
wahafidhina. Lakini kubwa zaidi ulikuwa ni uchaguzi kati ya wanaotaka Jamhuri
ya Watu wa Zanzibar yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa na wale vibaraka
wanaotaka Zanzibar iendelee kuwa koloni la Tanganyika. Umma ulipoonekana kuwa
upande wa wanaopenda maridhiano, wanaotaka maendeleo na wanaoitaka Zanzibar
yenye mamlaka kamili,
watawala wakijumuika kati ya vibaraka waliopo Zanzibar na
wakoloni wanaowatumikia wakaamua kutumia nguvu kubwa ili kujaribu sauti ya
nguvu hiyo isitoke.
Wasichokijua
ni sauti imetoka na imesikika, tena bila ya kisisi. Balozi Seif Ali Iddi (katika
comment moja jamaa alimwita Balozi wa Tanganyika nchini Zanzibar) na wenziwe
wanaotumikia agenda ya Tanganyika hapa Zanzibar walidhani kwa kutumia nguvu ile
kubwa watatuyumbisha na kutuhamakisha tuivunje Serikali ya Umoja wa Kitaifa
ambayo yeye na wenzake hawakuahi kuiamini wala kuiunga mkono na kwa kufanya
hivyo wakadhani watafanikiwa kuyavunja maridhiano na umoja wa Wazanzibari.
Wakadhani wakifanikiwa katika hilo watakuwa wamevunja umoja na ari ya
Wazanzibari kudai nchi yao. Wamepwerewa wao na mabwana wanaowatumikia. Akili
zetu razina. Haondoki mtu kwenye mstari. Tutayalinda maridhiano na umoja wa
Wazanzibari. Na tutalilinda na kulipeleka mbele vuguvugu la Wazanzibari
linalojumuisha makundi na taasisi tofauti kuirudisha Zanzibar yetu".
<
No comments:
Post a Comment