Friday, September 7, 2012

RAIS KIKWETE ATUNUKIWA TUZO LA KIMATAIFA LA KILIMO


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARIRAIS KIKWETE ATUNUKIWA TUZO LA KIMATAIFA LA KILIMO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametunukiwa Tuzo Maalum ya Sera za Usalama wa Chakula na Uongozi Katika Sekta ya Kilimo ikiwa ni ishara ya kuthamini mchango wake na uongozi wake katika sekta hiyo ya kilimo.
Tuzo hiyo imetolewa na Taasisi ya Mtandao wa Kutathmini Sera za Kilimo na Maliasili – Agriculture and Natural Resources Policy Analysis Network (FANRPAN) katika hafla maalum iliyofanyika jioni ya jana, Jumatano, Septemba 5, 2012, wakati wa mkutano wake wa mwaka unaofanyika kwenye Hoteli ya White Sands mjini Dar es Salaam.

Rais Kikwete anakuwa kiongozi wa tano wa Afrika kupokea Tuzo hiyo ambayo kwa lugha ya Kiingereza inajulikana kama Food Security Policy Leadership Award tokea kuanzishwa kwa Tuzo hiyo mwaka 2008 wakati ilipotolewa kwa aliyekuwa Rais wa Malawi, Hayati Bingu Wa Mutharika.
Viongozi wengine ambao wamepata kutunukiwa Tuzo hiyo ni Rais Armando Emilio Guebuza wa Mozambique mwaka 2009, Rais Hifikepunye Pohamba wa Nambia mwaka 2010 na Malkia, Mama wa Mfalme Ntombi, Indlovukazi wa Swaziland.Akizungumza mara baada ya kupokea Tuzo hiyo, Rais Kikwete aliwapitisha washiriki wa mkutano huo kwenye hatua zote ambazo Serikali yake inachukua kupambana na changamoto zote zinazokifanya kilimo cha Tanzania kubakia kwenye uduni ikiwa ni pamoja na kuongeza maeneo ya umwagiliaji, matumizi ya mbegu bora, matumizi ya madawa ya kuua wadudu, matumizi ya mbolea nyingi zaidi, uboresha wa miundombinu ya barabara vijijini, uimarishaji wa vikundi vya ushirika wa uzalishaji na upanuzi na uimarishaji wa masomo.

Imetolewa na
:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu.

Dar es Salaam
.
6 Septemba, 2012

No comments:

Post a Comment