Tuesday, January 10, 2012

MMOJA AFA KATIKA MSONGAMANO HUKO SAUZ


Mtu mmoja amekufa baada ya mkanyagano kutokea miongoni mwa umati wa watu waliokuwa wakitaka kujiandikisha katika chuo kikuu mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
"Kuna mtu mmoja amekufa," msemaji wa Chuo Kikuu cha Johannesburg Herman Esterhuizen amesema.
Mtu huyo aliyekufa inasemekana ni mama mzazi wa mmoja wa wanafunzi watarajiwa.
Zaidi ya wanafunzi 180,000 wanatarajiwa kukosa nafasi katika vyuo vikuu tisa vyenye hadi ya juu nchini Afrika Kusini mwaka huu, limesema gazeti la Times.

Ukosefu wa ajira

Inasemekana takriban wanafunzi 74,000 watashindwa kupata nafasi katika chuo kikuu cha Johannesburg pekee.
Ukosefu wa ajira umesababisha nafasi za vyuo kukosekana zaidi, anasema mwandishi wa BBC wa Afrika Kusini Andrew Harding.
Tukio la Jumanne limetokea wakati wanafunzi wakijipanga kusaka nafasi za mwisho chuoni hapo, msajili wa chuo hicho Marie Muller amekiambia kituo cha habari cha eNews channel.

Kujeruhiwa

Wanafunzi waliowasilisha maombi walisubiri usiku kucha na mkanyagano unadhaniwa kutokea mara tu lango kuu lilipfunguliwa saa moja na nusu saa za Afrika Kusini, amekaririwa msemaji wa huduma za dharura Nana Radebe akisema.
Watu wawili pia wametajwa kujeruhiwa sana.
Wilson Matiba alikuwepo kwenye mkanyagano.
"mambo yaliharibika kabisa," alisema, akikaririwa na mtandao wa Mail & Guardian.

Usiku kucha

"Tulikimbilia kwenye lango kuu na watu walianguka. Hatukuweza kusimama," Amesema Bw Matiba, ambaye anajaribu kutafuta nafasi ya kusoma shahada ya sayansi katika Zoolojia.
Bw Matiba amesema wanafunzi wanaotafuta nafasi wanazitaka sana nafasi hizo na hawakuwa na muongozo wowote zaidi ya kuvamia lango kuu.
"Tunahitaji elimu, tunahitaji kujisajili. Tulihijati kuingia ndani," alisema.
Mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo - ambaye hakutaka kutajwa jina lake - alisema watu walisafiri kutoka maeneo mbalimbali nchini humo, wakisafiri usiku kucha kufika chuo hapo.
Alisema kulikuwa na tukio kama hili siku ya Jumatatu, na hali hiyo ilipotokea tena siku ya Jumanne "tulikimbia kwa sababu tulifahamu tungeweza kuumia".
Chuo Kikuu cha Johannesburg kinaripotiwa kuwa moja ya chuo ambacho kinachukua maombi yaliyochelewa katika mwezi wa Januari, baada ya matokeo ya mitihani ya shule ya sekondari kutoka na baadhi ya wanafunzi kufahamu kuwa wana nafasi ya kwenda chuo kikuu.
Siku ya Jumatatu, ambayo kwa kawaida huwa ni tulivu katika maeneo ya chuo kikuu hicho, badala yake magari yamejaa kwa umbali wa takriban kilomita moja kutoka katika lango kuu.

No comments:

Post a Comment