Maelfu ya raia wa Libya wameandamana katika jiji kuu Tripoli kulalamikia
makundi ya waasi ambao walisaidia kumuondoa madarakani Kanali Muammar
Gaddafi.
Raia hao waliopeperusha bendera walikusanyika katika medani ya
Martyrs ambapo walitaka utawala wa sasa kuwapokonya silaha wapiganaji
wote ambao wamekuwa wakidhibiti maeneo kadhaa ya jiji kuu.
Kumekuwa na makabiliano kati ya makundi hasimu na serikali iliwataka wapiganaji hao kuondoka Tripoli katika muda wa wiki mbili.
Waliandamana baadhi wakipeperusha bendera,
wengine matawi ya zeituni. Kundi moja la watoto walikuwa wamebeba
mabango yaliyosema "usiangamize mustakabali wetu". "hatutaki silaha,"
walisema.
Waasi ambao mwezi wa Agosti walipigana vita hadi
wakafika jijini Tripoli na kumuondoa madarakani Muammar Gaddafi sasa
hawakaribishwi tena hapa baada ya kuzuka makabiliano kati ya makundi
hasimu ya wapiganaji
Na katika jiji lisilo na kikosi rasmi cha jeshi
wala maafisa wa polisi , huku silaha zikiwa mikononi mwa wengi raia wa
eneo hili wamekerwa na kuzorota kwa hali ya usalama.
Mapema leo, majaji na mawakili waliandamana
baada ya wapiganaji waliojihami kwa silaha kujaribu kumlazimisha
mwendesha mashtaka kutia saini karatasi za kuwaachilia huru wapiganaji
wenzao waliofungwa jela.
Nao madaktari na wauguzi waliangalia tu wasijue
la kufanya baada ya wapiganaji wawili waliojihami na bunduki kuvunja
milango na kumtoa nje kwa nguvu aliyesimamia hospitali , wakipinga vile
mgonjwa mmoja alihudumiwa.
Na katika chumba cha wagonjwa mahututi kumejaa
watu ambao wa majeraha ya risasi. Hali katika hospitali imezidi kuwa
mbaya baada ya baada ya madaktari kutoroka wakitaka kuhakikishiwa
usalama wao na serikali.
No comments:
Post a Comment