Monday, December 26, 2011

KHALIL IBRAHIM AUAWA

Jeshi la Sudan linasema kuwa limemuuwa kiongozi wa kundi lenye nguvu kabisa katika jimbo la Darfur, kundi la Justice and Equality Movement, yaani JEM.
Khalil Ibrahim, kiongozi wa JEM
Ikithibitishwa, basi kifo cha Khalil Ibrahim kitakuwa pigo kubwa kwa chama chake cha JEM.
Bwana Ibrahim alianzisha kundi hilo na kulijenga hadi kuwa na nguvu kubwa na silaha nyingi kabisa katika jimbo la magharibi la Sudan, Darfur.
JEM ilihusika na mashambulio makubwa; pamoja na lile la mwaka wa 2008, ambapo ilifanya shambulio katika mji mkuu, Khartoum.
Watu 220 waliuwawa, wakati wapiganaji wa JEM waliposafiri kwa magari jangwani hadi kufika Omdurman, ambayo iko ng'ambo ya pili ya Mto Nile, mkabala na ikulu ya rais.
Wanajeshi wa serikali waliwatimua baada ya mapambano makali.
Kanali Gaddafi alimpa hifadhi kiongozi wa JEM, na kumsaidia kifedha na kijeshi.
Lakini baada ya Kanali Gaddafi kuondolewa madarakani, Khalil Ibrahim alikimbia Libya kurejea Sudan.
Alitia saini na serikali ya Sudan mwezi wa Februari ya kusitisha mapigano, lakini alitoka kwenye mazungumzo ya amani punde baadae.

No comments:

Post a Comment