Friday, June 1, 2012

TEMBO MTABIRI MATOKEO.... NI BAADA YA KIFO CHA PWEZA PAUL



Tembo mmoja nchini Poland anatarajiwa kuchukua nafasi ya Pweza Paul kwa kutabiri matokeo ya michuano ya maataifa ya Ulaya yanayoanza hivi karibuni.
Tembo huyo anayejulikana kama Citta mwenye umri wa miaka thelathini na mitatu atakuwa akitumia mkonga wake kubashiri timu itakayoshinda.
Habari kutoka Warsaw zinasema ubashiri wa kwanza utafanywa tarehe sita mwezi Juni, siku mbili kabla ya kuanza kwa michuano hiyo. Tembo huyo alifanya kituko wakati akitambulishwa kwa waandishi wa habari, baada ya kuumeza mpira wa miguu uliokuwepo mezani.
Mkurugenzi wa hifadhi ya wanyama ya mjini Warsaw Teresa Grega amesema tembo huyo alitabiri ushindi wa Chelsea dhidi ya bayern Munich katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya hivi karibuni. Tembo huyo atatabiri mshindi kati ya Poland watakaopambana na Ugiriki Juni nane.
Atapewa matunda matatu, mawili yakiwa na majina ya timu hizo mbili, na tunda la tatu kwa ajili ya kutabiri sare. Tembo huyo alizaliwa India, akaishi Ujerumani kabla ya kwenda Austria, halafu Uhispania na hatimaye kuhamia Poland. Bi Gregga amesema tembo huyo anapenda sana kutazama soka.

No comments:

Post a Comment