Monday, May 28, 2012

KUTAPATAPA MAWAZIRICHANZO MWANANCHI


KATIKA siku za hivi karibuni umeanzishwa utamaduni wa ajabu katika nchi yetu, ambapo mawaziri wanaoondolewa au kuachwa katika Baraza la Mawaziri wanakimbilia katika majimbo yao ya uchaguzi siyo tu kwa lengo la kupata huruma ya wapigakura , bali pia kujenga dhana kwamba kutemwa kwao na mamlaka iliyokuwa imewateua kumetokana na fitina na  wivu wa washindani wao kisiasa katika chama tawala na serikali yake.

Pengine yafaa tukumbushane hapa kwamba utamaduni huo wa ajabu uliasisiwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na kufuatiwa na Edward Lowassa aliyelazimika kuachia kiti cha uwaziri mkuu. Hali hiyo imeshika kasi hivi sasa baada ya mawaziri William Ngeleja, Ezekiel Maige, Omari Nundu, Cyril Chami na Mustafa Mkulo kuondolewa katika nyadhifa zao. Ni Dk Haji Mponda pekee aliyeachishwa uwaziri  pamoja na wenzake hao watano hivi karibuni lakini akaamua kukaa kimya. <

Hayo ndiyo matokeo ya kutojifunza kutokana na historia, kwa maana kwamba watu hao walioachishwa uwaziri walishindwa kutambua kuwa, hawakuwa mawaziri wa kwanza kupokonywa nyadhifa zao hizo. Tunadhani wangefanya vyema iwapo wangetambua kwamba cheo ni dhamana tu, hivyo hawatazamiwi kutaharuki  pindi mwenye dhamana yake anapoamua kuichukua. Hivyo ndivyo walivyofanya watangulizi wao, wakiwamo Iddi Simba, Juma Ngasongwa, Simon Mbilinyi na Ali Hassan Mwinyi ambaye alikuja kuchaguliwa katika vipindi tofauti kuwa Rais wa Zanzibar na baadaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
    
Mawaziri wanaoondoshwa na kupatwa ghadhabu na mfadhaiko kama hao tuliowataja wanashindwa kuelewa kwamba waliomba ubunge na siyo uwaziri, hivyo aliyewapa uwaziri huo anaweza kuuchukua pasipo kulazimika kutoa maelezo. Ni jambo la kushangaza kuona kuwa, baadhi ya mawaziri hao waliong’olewa wametoa vitisho kadhaa, ikiwa ni pamoja na kwamba wafuasi wao watahamia kambi ya upinzani.

No comments:

Post a Comment