Salum Maige, Sengerema
MLINZI wa Kampuni ya Mass Security Gambeta
amefanikiwa kupambana na watu saba wanaodhaniwa kuwa majambazi na kumwua
mmoja kisha kuwapora bastola.
Mauaji hayo yalitokea baada ya
zaidi ya dakika 30 za kurushiana risasi baina ya mlinzi huyo na
majambazi hayo, yaliyotokea katika maduka ya kijiji cha Mbugani
kilichoko kwenye Kata ya Bulyaheke wilayani Sengerema, Mwanza.
Katika
mapambano hayo mlinzi huyo alifanikiwa kumpiga risasi ya mguuni mmoja
wa majambazi hao na kuanguka na kumchapa mwingine risasi iliyomfanya
aangushe bastola na kukimbia.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji
cha Mbungani, Msiba Etangi alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia
juzi Jumamosi majira ya saa nane usiku, wakati majambazi hayo
yakijiandaa kuiba katika maduka ya wananchi wa kijiji hicho yanayolindwa
na kampuni hiyo.
Jambazi lililouawa limetambulika kwa jina moja
la Juma linakadiriwa kuwa na umri usiozidi miaka 28 na kwamba makazi
yake yako jijini Dar es Salaam lakini awali linadaiwa lilikuwa likiishi
wilayani Geita mkoani Mwanza.
Mwenyekiti alifafanua kuwa jambazi
hilo baada ya kupigwa risasi na kuanguka chini lilikutwa na bunduki
moja aina ya SMG na kwamba kabla ya kukata roho liliwataja baadhi ya
watu waliokuwa wakishirikiana nalo katika tukio hilo baadhi yao wakiwa
wakazi wa kijiji hicho na wengine wa kijiji jirani cha Kanyala.
''Majambazi
hayo yalikuwa na bunduki, mapanga, marungu na jiwe kubwa fatuma na
yalikuwa yakijiandaa kupora kwenye moja ya maduka ya hapa, lakini mlinzi
alipobaini kuwa ni wahalifu alipambana nayo kwa muda wa dakika 30 na
akawa amelipiga limoja risasi miguuni na kuanguka. Baada ya kulipekuwa
tumekuta likiwa na bunduki moja SMG ambayo nafikiri lilikuwa likitumia
wakati wa mapambano na mlinzi huyo,'' alisema.
Kamanda wa Polisi
mkoani Mwanza, Liberatus Barrow alipotafutwa kwa njia ya simu
kuzungumzia tukio hilo alisema hana taarifa na kuahidi kuongea na
wasaidizi wake ili apate taarifa zaidi kama kuna tukio kama hilo''.
Kwa
upande wake kamanda wa Polisi Wilaya ya Sengerema, OCD Pundensiana
alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo alisema yeye sio mzungumzaji licha
ya kukiri kuwepo kwa tukio hilo na kwamba alituma askari wake eneo la
tukio kufuatilia.
''Ndugu yangu mimi sio msemaji lakini tukio
hilo lipo, nafikiri hebu mpigie aliyekupa hizo taarifa akupe maelezo
jinsi tukio lilivyotokea, lakini nimetuma askari kufuatilia na kufanya
uchunguzi kwa hiyo na wewe fuatilia,'' alisema.
Hata hivyo
mwenyekiti wa kijiji hicho, Etangi alisema watu wanne waliotajwa na
jambazi hilo kabla ya kukata roho walikamatwa na polisi waliokuwa
wamefuatilia tukio hilo kwa amri ya kamanda wa polisi Sengerema.
No comments:
Post a Comment