ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yussuf Makamba amejitokeza hadharani kwa mara ya kwanza na kuzungumzia mustakabali wa taifa kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Makamba amekuwa kimya kwenye ulingo wa siasa, tangu alipoondolewa kwenye nafasi ya Ukatibu Mkuu ndani ya CCM alisema Watanzania waamini kuwa Mgombea urais 2015 atatoka kwa Mungu.
Makamba alisema amesikia kelele nyingi kuhusu nani akayemrithi Rais Jakaya Kikwete lakini pamoja na hayo yote atakayeamua hatma ya mgombea urais ni Mungu peke yake.
Mwanasiasa huyo machachari, anayesifika kwa kwa kutolea mifano maandiko ya kwenye vitabu vya biblia na quran, alikwenda mbali zaidi na kunukuu maandiko ya biblia akisema; “ Si kila mtu aniitae bwana bwana atakayeurithi ufalme wa mbinguni’ akiwa na maana kuwa si wote wanaoutaka urais watakuwa marais.
Akitolea mfano, Makamba alisema hata wakati Kanisa la Kiinjili ya Kiluteri Tanzania (KKT) wanamchagua Askofu Mkuu wao Maaskofu wawili waliokuwa wakigombea nafasi hiyo, Steven Munga wa Dayosisi ya Lushoto na Askofu Owdenberg Mdegella wa Dayosisi ya Iringa baada ya kupigiwa kura kwa takribani mara tatu walishindwa kumpata mgombea.
“Lakini aliibuka askofu mmoja akasema tuongeze jina la Alex Malasusa, jina la Malasusa lilipoongezwa tu walipopiga kura mara moja, Malasusa akapita, hivyo nataka kuwaambia kuwa mgombea urais 2015 atatoka kwa Mungu na atapatikana kwa staili kama aliyopatikana Malasusa…hivyo watu wasiwe na mashaka” alisema Makamba.
Baadhi ya wanasiasa wanaotajwa kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Afrika Mashariki, Bernad Membe.
Wengine ni Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, John Nchimbi.
Alipoulizwa kati ya wanaotajwa kuwania kiti cha urais 2015 ni yupi ambaye anamuunga mkono, Makamba alisema ni mapema mno kuweka msimamo wake wazi.
Hata hivyo alisema muda ukifika na mchakato wa kuchukua fomu za kuwania urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi utakapoanza na baada ya wagombea kuchukua fomu ndipo atakapotangaza mgombea anayemuunga mkono.
Katika hilo, alisema mgombea atakayemuunga mkono yeye ana uhakika atapita na ndiye atakayeshinda urais 2015.
Makamba ambaye ni mwanasiasa machachari mwenye maneno mengi, akizungumzia hilo alikwenda mbali zaidi na kutahadharisha kuwa mgombea atakayeungwa mkono na Rais Jakaya Kikwete kugombea urais 2015 ataanguka.
Alisema mgombea atakayebebwa na Rais Kikwete yatampata kama yaliyompata Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2002 alibebwa na Rais Daniel arap Moi awe mgombea wa KANU lakini matokeo yake chama kikamegeka na kusambaratika na Mwai Kibaki aliyekuwa akigombea kupitia chama cha Upinzani akaibuka mshindi kwa kura nyingi.
Uhuru ambaye ni mtoto wa Rais wa kwanza wa Kenya alichaguliwa kuingia bungeni mwaka 2001, na kuteuliwa kuwa Waziri wa Serikali za Mitaa chini ya utawala wa Rais Moi na pamoja na kwamba hakuwa na uzoefu mkubwa wa kisiasa Rais Moi alikuwa akitaka awe mrithi wake.
Mbali na hilo Kuhusu CCM na harakati zake za siasa kuelekea uchaguzi Mkuu wa 2015, Makamba ambaye amepata kuwa kiongozi ndani ya CCM akianzia nafasi ya chini na kupanda hadi kushika nyadhifa za juu kabisa alisema ana uhakika chama hicho kitashinda.
Alipinga akisema kuwa chama hicho hakina makundi kama ambavyo baadhi ya watu wanatafsiri.
“Nimekaa CCM kwa muda mrefu sana…sijaona makundi yanayosemwa, ila kama ukisema pale ambapo wagombea wanachukua fomu za kuwania urais, hapo sawa makundi lazima yaibuke kwa sababu kila mmoja kuna mtu wake ambaye anaona anafaa kuwa rais” alisema Makamba.
Kuhusu dhana ya ‘kujivua gamba’ ndani ya CCM, Makamba alisema kauli hiyo imetafsiriwa vibaya na wale wanaoitekeleza.
Alisema lengo la kujivua gamba halikuwa likiwalenga baadhi ya wanasiasa wachache ndani ya Chama cha Mapinduzi wanaotuhumiwa kwa ufisadi bali ililenga kuwaondoa watu walioonekana kukaa kwa muda mrefu katika safu za uongozi ndani ya chama na kuleta damu changa ili nao waje waongoze wakiwa na mbinu mpya.
Alisema dhana hiyo imepotoshwa na wale wanaoitekeleza wanaitekeleza kwa malengo tofauti.
Source: Gazeti la Fahamu
No comments:
Post a Comment