Sunday, May 27, 2012

YAKUBU AIKIMBIA BLACKBURN


Mchezaji wa kimataifa wa Nigeria, Yakubu Aiyegbeni, huenda alimalizana na Blackburn Rovers msimu uliokwisha, baada ya klabu hiyo kushushwa daraja.
Mchezaji huyo, mwenye umri wa miaka 29, ameilezea BBC kwamba kamwe hataki kucheza mechi katika kiwango cha Championship.
Yakubu alikuwa ni kati ya wachezaji waliong’ara katika timu ya Blackburn, na alifunga jumla ya magoli 18.
Ana miaka miwili katika mkataba wake, lakini bila shaka kuna vilabu vingi ambavyo vinaweza kuhitaji huduma za mshambulizi wa kiwango hicho.
Yakubu aliwahi pia kuvichezea vilabu vya Everton na Middlesbrough katika ligi kuu ya England.
Msimu uliopita, atakumbukwa kwa kufunga magoli mawili dhidi ya Manchester United, wakati Blackburn ilipopata ushindi wa magoli 3-2 mwezi Desemba.
Yakubu Aiyegbeni
Huenda akaihama Blackburn
Aliifungia Blackburn thuluthi moja ya magoli yote ya klabu hiyo.
Ingawa aliwahi kucheza katika Championship wakati alipokuwa mchezaji wa Leicester City, kamwe hana mipango kucheza katika soka ya kiwango cha chini.
“Ilikuwa ni nzuri, lakini sitaki kucheza tena huko”, alielezea.
Matamshi hayo hayatamshangaza meneja Steve Kean, ambaye bila shaka anatambua Yakubu huenda akavutiwa kucheza soka katika vilabu vingine, na tayari QPR na Reading, ambayo imepandishwa hadhi, wakiwa tayari wamevutiwa naye.
Wakati huohuo Yakubu anatambua ni Blackburn iliyomsaidia kujiimarisha tena, baada ya Everton kukosa imani naye, na kumuazima kwa timu ya Leicester.
"Mashabiki na wachezaji wa Blackburn ni watu wazuri mno. Bila wachezaji hao, nisingeliweza kuwa na msimu wenye fanaka," aliongezea.
"Walinipa nafasi ya kurudi katika ligi ya Premier na kuonyesha uwezo wangu, wiki baada ya wiki."
Yakubu kwa hivi sasa yuko nchini Zimbabwe kushiriki katika mechi huko, kufuatia mwaliko wa mchezaji mwenzake aliyecheza naye katika klabu ya Portsmouth, Benjani Mwaruwari.
Ni kati ya wachezaji kadha waliobobea katika timu ya taifa ya Nigeria na ambao hawamo katika kikosi kilichochaguliwa kucheza mechi za kimataifa, ikiwa ni pamoja na John Obi Mikel, Peter Odemwingie na Taye Taiwo.

No comments:

Post a Comment