Ben Komba/Pwani-Tanzania/17-May-12/05:29:34 PM
Zaidi ya shilingi milioni 455 zitatumika katika ujenzi wa jengo la
chama cha walimu mkoa wa Pwani, ikiwa ni moja ya majengo yanayokusudiwa
kujengwa kila mkoa katika kuhakikisha chama hicho kinajiimarisha
kiuchumi kwa kujenga vitega uchumi ambavyo vitaongeza kipato na usalama
wa maisha ya Mwalimu mara baada ya kustaafu utumishi.
Katibu wa Chama cha Walimu
Mkoa wa Pwani, MWL. NEHEMIAH JOSEPH amemweleza mwandishi wa habari hizi
ofisini kwake mjini Kibaha kuwa chama chao kinategemea kukamilika kwa
ujenzi wa jengo lao la ghorofa mbili ambalo linajengwa na kampuni ya
SUMA JKT katika mwezi Septemba, ambapo litakapokamilika jengo hilo
litakuwa na ofisi za chama cha walimu mkoa na wilaya, Benki ya walimu,
ukumbi wa mikutano na ofisi nyingine zitapangishwa kwa wahitaji.
MWL. JOSEPH ameongeza mradi huo wa kujenga ofisi utaendelea mpaka ngazi
ya wilaya ambapo mpaka sasa katika mkoa wa Pwani wilaya ambazo zina
ofisi zao wenyewe ni wilaya ya Rufiji ofisi yake imeshakamilika, wilaya
ya Bagamoyo na Kisarawe ofisi zao zipo katika hatua za mwisho kuelekea
katika kukamilika.
MWL. NEHEMIAH JOSEPH amefafanua mpaka sasa
wilaya ambazo hazina ofisi lakini zipo katika mchakato wa kujenga ofisi
zao ni Mkuranga, Mafia na Kibaha ambao bado wanatafuta kiwanja, ujenzi
huo ni mafanikio ya Jengo la Mwalimu HOUSE ambapo kupitia kitegauchumi
hicho chama chao kimekuwa na kiu ya kufanya vizuri kutokana na mapato
yanayopatikana na MWALIMU HOUSE kutumika kujenga ofisi katika kila mkoa.
Aidha ameongeza sehemu kubwa ya fedha za ujenzi wa ofisi za Chama cha
walimu katika kila mkoa ni nguvu za walimu wenyewe na hakuna mfadhili wa
nje wala wa ndani anayewasaidia katika utekelezaji wa mradi huo maalum
wa kujenga ofisi katika kila mkoa, ambapo katika ofisi hizo kutakuwa na
eneo kwa ajili ya Benki ya walimu ambayo itakuwa inatoa fursa ya mikopo
kwa wanachama walimu kwa riba ndogo katika kumuwezesha Mwalimu kumudu
hali ya maisha na kujitegemeza kiuchumi.
Katibu huyo wa chama
cha walimu mkoa wa Pwani (CWT), MWL. NEHEMIAH JOSEPH ametoa wito kwa kwa
walimu kujenga umoja na mshikamano miongoni mwao ili kujenga msingi
imara ambao hautatetereshwa na kitu chochote kwa kuunganisha nguvu zao
katika kujiimarisha kiuchumi.
END.
No comments:
Post a Comment