Wednesday, May 23, 2012

TCRA WALONGAA

na Sitta Tumma, Kwimba

MAMLAKA ya Mawasiliano Nchini (TCRA), imesema mionzi na mawimbi ya mawasiliano ya simu hayana madhara kwa watumiaji, tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya watu.
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Lawi Odiero, alisema katika kubaini ukweli huo walifanya utafiti, ili kufahamu iwapo kuna athari kubwa ambazo zinaweza kumdhuru mtumiaji, jambo ambalo imebaini hakuna athari zozote zinazoweza kujitokeza, badala yake simu yenyewe huchemka iwapo mtumiaji atatumia muda mrefu kuzungumza kwa wakati mmoja.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mawasiliano na Teknolojia yaliyofanyika Mei 17 kwenye shule ya sekondari ya wasichana ya Bishop Mayala iliyo kijiji cha Ibindo, meneja huyo aliwataka Watanzania kuendelea kutumia mawasiliano ya simu, kwa maendeleo yao, na kwamba mamlaka hiyo imejizatiti kuhakikisha inaboresha zaidi utoaji wa huduma zake.
“Mionzi ya mawasiliano ya simu haiwezi kumdhuru mtumiaji kama ambavyo imekuwa ikielezwa. Isipokuwa mtumiaji anayezungumza muda mrefu kwa wakati mmoja simu hupata joto,” alisema.
Pamoja na mambo mengine alisema mamlaka hiyo imejiimarisha zaidi katika suala zima la kukuza na kulinda mawasiliano kwa maslahi ya watumiaji nchini, ikiwa ni pamoja na kuendelea kutekeleza mikataba mbalimbali ya kimataifa katika kuleta ufanisi bora wa huduma ya mawasiliano kwa Watanzania.

No comments:

Post a Comment