Wednesday, May 16, 2012

Poulsen achagua timu

Kocha mpya wa timu ya taifa ya Tanzania bara, Kim Poulsen, amekosa kuwachagua katika kikosi chake baadhi ya wachezaji wa muda mrefu wa timu ya taifa.
Kim Poulsen
Kocha mpya amekosa kuwachagua baadhi ya wachezaji wazoefu
Poulsen, kutoka Denmark, amewachagua wachezaji wapya kuwa miongoni mwa wachezaji 22 wa timu ya Taifa Stars.
Juhudi hizo ni miongoni mwa maandalizi ya kocha huyo kwa mashindano ya kufuzu kwa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014.
Ameamua kuwatema baadhi ya wachezaji wenye uzoefu wa muda mrefu na kuwachagua vijana wadogo zaidi.
"Nimeamua kuwachagua vijana hawa wadogo kwa kuwa ninaamini wataweza kuifanya kazi hiyo ya timu ya taifa", alielezea.
Kikosi cha Tanzania kina wachezaji;
Kipa: Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ally (Azam), Deogratius Munishi (Mtibwa Sugar)
Walinzi: Nassor Masoud Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Simba), Waziri Salum (Azam), Shomari Kapombe (Simba) na Juma Nyoso (Simba)
Kiungo cha Kati: Mwinyi Kazimoto (Simba), Salum 'Sure Boy' Abubakar (Azam), Nurdin Bakari (Yanga), Jonas Mkude (Simba), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Edward Christopher (Simba), Mrisho Ngasa (Azam) Frank Domayo (JKT Ruvu)
Washambulizi: Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu (both TP Mazembe, DR Congo), Ramadhan Singano (Simba), Simon Msuva (Moro United), Haruna Moshi (Simba), John Bocco (Azam)
Poulsen aliwahi kuifunza timu ya Tanzania ya vijana chini ya umri wa miaka 17 na vile vile miaka 20, kabla ya kurithi kazi ya raia mwenzake wa Sweden, na ambaye majina yanafanana, Jan Poulsen.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 52 ameamua kutowaalika wachezaji wa zamani kama nahodha Shadrack Nsajigwa, Nadir Haroub, Henry Joseph, Nizal Khalfan na Abdi Kassim.
Kinyume na hayo, ameamua kumchukua tena mshambulizi mwenye umri mdogo Mbwana Samata, ambaye huichezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, na ambaye alikuwa ametupwa nje na kocha wa awali Jan Poulsen.
Wachezaji wengine walioalikwa kujiunga na timu ya taifa kwa mara ya kwanza miongoni mwa vijana waliopo katika timu ya chini ya umri wa miaka 20 ni pamoja na Ramadhani Singano, Edward Christopher na Frank Domayo.
"Kuna matumaini siku zijazo kupitia timu hii, na ninaamini mchezo wao utastawi na kustawi", alielezea Poulsen.
Kikosi kitaanza mazoezi yake kikiwa kambini kuanzia Jumatano, kwa nia ya kujiandaa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Malawi, tarehe 26 mwezi huu wa Mei.

No comments:

Post a Comment