MANCHESTER, England
KOCHA wa Manchester City, Roberto Mancini amesema
anatarajia uongozi wa klabu yake utamruhusu kutumia fedha nyingi kwa
ajili ya usajili wa msimu ujao wa Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa.
Mancini
hivi sasa mpango wake ni kuhakikisha anakuwa na kikosi bora ili achukue
ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu
ya England.
Mpaka sasa Man City imeshatumia fedha nyingi kwa
wachezaji walioiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa England tangu timu
hiyo ilipochukuliwa na tajiri wa Abu Dhabi, Sheikh Mansour mwaka 2008.
Kwa
upande wa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Khaldoon al-Mubarak yeye alisema
hakuna haja ya kutumia fedha nyingi hivi sasa kwa ajili ya usajili kwa
sababu Man City ina kikosi imara, lakini kocha Mancini yeye anataka
kununua wachezaji wengine wenye majina makubwa.
Mancini
alisema,"Barcelona na Real Madrid kila mwaka zinanunua wachezaji wawili
au watatu na zinatumia fedha nyingi, nafikiri Manchester City na yenyewe
itakuwa hivyo."
Alisema,"inabidi kuboresha kikosi, tunahitaji nguvu zaidi kucheza Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu ya England."
Katika misimu miwili iliyopita klabu za Real Madrid na Barcelona zilitumia kiasi cha pauni 105 milioni kwa ajili ya usajili.
Barcelona
ilimnunua David Villa kwa pauni 34.2 milioni mwaka 2010 na miezi 12
baadaye walitumia kiasi kama hicho kumnunua Cesc Fabregas.
Madrid
wenyewe tangu mwaka 2009 walimsajili Cristiano Ronaldo kwa pauni 80
milioni pia Kaka na Karim Benzema walisajiliwa kwa kiasi cha pauni 170
milioni kwa pamoja.
Mwaka jana Man City ilitumia kiasi cha pauni
197 milioni kufanya usajili, lakini mwaka huu inataka kutumia pia fedha
nyingi kwa sababu inataka kumsajili mshambuliaji wa Arsenal, Robin Van
Persie na kiungo wa Lille, Eden Hazard.
"Tunatakiwa kuwa na
kikosi imara kwa sababu mwaka wa kwanza tulichukua kombe la FA, mwaka wa
pili tumechukua ubingwa wa Ligi Kuu, mwaka wa tatu tunatakiwa kuchukua
ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya,"alisema Mancini.
Mancini hivi
karibuni pia anatarajiwa kuanza mazungumzo mapya na uongozi wa
Manchester City kwa ajili ya kuongeza mkataba wa kuendelea kuinoa timu
hiyo.
No comments:
Post a Comment