KIPA wa timu ya Moro United, Jakson Chove amesema ni kama Patrick
Mafisango alijitabiria kifo kutokana na mambo aliyofanya saa chache
kabla ya kifo chake katika ukumbi wa Maisha Club uliopo Oysterbay jijini
Dar es Salaam na kabla ya hapo.
Akizungumza na Mwananchi
nyumbani kwa mshambuliaji Emmanuel Okwi unapofanyika msiba wa Mafisango,
kipa Chove alisema Mafisango ni rafiki yake mkubwa ambaye
walifahamiana tangu wakiwa Ruanda ambako walikuwa wakicheza soka wote.
Alisema
ukiacha maisha ya soka, Mafisango kwake ni zaidi ya ndugu kwani alikuwa
ni mtu wake wa karibu na mara ya mwisho waliwasiliana muda mfupi kabla
ya kupata ajali iliyochukua maisha yake.
"Nilizungumza na
Mafisango akinitaka niende Maisha Club nikaagane naye kabla ya kwenda
kwao ambako ameitwa kwenye timu ya Taifa ya Rwanda,"alisema Chove.
Alisema,"alinighasi
sana mchana kutwa akitaka tuonane na alipoona simjali akaniambia
niagizie chakula sehemu ambayo huwa tunakula na alinitumia fedha kwenye
simu ili nilipe kabisa, nilifanya hivyo, lakini baada ya hapo
niliondoka, ambapo Mafisango alipofika kula hakunikuta kitu
kilichomfanya anitukane sana kwenye simu."
"Sielewi niseme nini
kwa kuwa kifo hakikwepeki Mafisango alinibembeleza sana nionane naye
jana, lakini nilikuwa mzito si ajabu ningekuwepo haya yasingetokea kwa
kuwa mara nyingi akiwa amekunywa huwa namuendesha hadi kwake na baadaye
napanda daladala narudi kwangu,"alisema Chove.
Akielezea jinsi
alivyopata habari za msiba huo alisema baada ya kuona anamsumbua sana
akimtaka aende Maisha Club ilibidi azime simu na alipoiwasha muda wa saa
10 na nusu alfajiri akapigiwa simu na mwanamuziki wa FM Academia
aitwaye Hitler na kumuuliza kama amenusurika akiamini alikuwa naye.
"Nikashangaa
nimenusurika nini ndio akaniambia kuwa Mafisango amefariki dunia kwa
ajali ya gari, sikuamini, hata sasa siamini najilazimisha
kuamini,"alisema Chove.
Aliendelea kusema kuwa Hitler alimpigia simu na kumwambia kuwa Mafisango ni kama kajitabiria kifo chake.
Akielezea
kile alichokifanya Mafisango ukumbini hapo, mwanamuziki Hitler wa
kundi la FM Academia alisema Mafisango alikuwa amechangamka sana na mara
nyingi alikuwa akipanda jukwaani kutunza fedha kama wafanyavyo
'mapedeshee'.
"Alinipa cheni ambayo alisema ina thamani kubwa na
kuniambia ni kumbukumbu yangu nitamkumbuka sana nikiitazama cheni hiyo,
sasa kwangu hayo ni mambo ya ajabu kwa Mafisango ingawa ni mpenzi wa
bendi hii, lakini haya aliyofanya ni mapya kabisa,"alisema Hitler.
Chove
aliendelea kusema kuwa alijuana na Mafisango tangu wapo Ruanda ambapo
hata alipokuwa akitoka JKT kujiunga na Azam viongozi walimuuliza kuhusu
mchezaji huyo kama anamjua na mazungumzo ya kwanza ya kujiunga na timu
hiyo ni yeye ndio alifanya naye.
"Kabla ya kujiunga na Azam mimi
ndio nilifanya mazungumzo naye kwanza kabla ya viongozi kwa kuwa
waliniuliza uwezo wake kwani ndio nilikuwa natoka Rwanda hivyo nilikuwa
namfahamu tangu huko,"alisema kwa uchungu Chove.
No comments:
Post a Comment