Tuesday, January 24, 2012

Syria yakataa kujiuzulu kwa Assad




Syria imekataa pendekezo la Jumuiya ya Kiarabu la kutaka Rais Bashar al-Assad kumkabidhi madaraka naibu wake.
Jumuiya hiyo, inayokutana mjini Cairo, inataka Syria kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na upinzani katika muda wa miezi miwili ijayo.

Umoja wa Mataifa unasema watu zaidi ya 5,000 wamefariki dunia kutokana na serikali kukabiliana na waandamanaji tangu kuanza kwa maandamano mwezi wa tatu,mwaka uliopita.Afisa wa serikali ameuita mpango huo kama "kuingilia masuala ya ndani '' ya Syria, Televisheni ya taifa ilisema.
Jumuiya hiyo imetaka pande zote mbili kusitisha mapigano.
Serikali ya mjini Damascus inasema inakabiliana na "magaidi na magenge yenye silaha" na kudai kuwa maafisa 2,000 wa usalama wameuawa.

Mgawanyiko katika Jumuiya ya nchi za Kiarabu

"Syria imekataa uamuzi uliochukuliwa ambao ni nje ya mpango wa Jumuiya ya Kiarabu, na inachukulia hilo kama kuingiliwa kwa uhuru wake pamoja na mambo yake ya ndani," afisa mmoja wa serikali ya Syria ambaye hakutaka jina lake kutajwa alisema.
Afisa huyo alisema kuwa mapendekezo ya Jumuiya ya nchi za Kiarabu hayazingatii maslahi ya raia wa Syria na hayatozuia nchi hiyo "kuendeleza mchakato wake wa mabadiliko ya kisiasa na kuleta amani na usalama kwa watu wake".
Nchi ya Saudi Arabia inasema inaondoa wajumbe wake katika kundi la waangalizi 165 nchini Syria kwa kuwa Damascus imevunja ahadi yake ya kuendeleza mchakato wa amani.

No comments:

Post a Comment