Monday, January 23, 2012

ICC kutoa uamuzi kuhusu washukiwa Kenya


Mahakamani icc
ICC itaamua jumatatu kuhusu mstakabali wa washukiwa wa ghasia za Kenya.
Mahakama ya kimataifa ya jinai,ICC iliyoko mjini The Hague, Uholanzi, itaamua jumatatu ikiwa naibu waziri mkuu wa Kenya Uhuru Kenyatta pamoja na watu wengine watano mashuhuri wana kesi ya kujibu kuhusiana na tuhuma dhidi yao za kuhusika katika ghasia zilizoikumba nchi hiyo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 ambapo zaidi ya watu 1,300 waliuwawa.
Washukiwa wengine ni aliyekuwa waziri wa elimu ya juu William Ruto, aliyekuwa waziri wa viwanda Henry Kosgey, mkuu wa utumishi wa umma Francis Muthaura, aliyekuwa mkuu wa Polisi Generali Hussein Ali na mtangazaji wa redio Joshua Arap Sang.
Kwa mujibu wa taarufa kutoka ICC, jopo la majaji watatu linaloongozwa na Ekaterina Trendafilova litawasilisha uamuzi wao kwa watuhumiwa na mawakili wao kwanza kupitia maandishi, kisha saa tano na nusu kwa saa za mjini The Hague, ambayo ni sawa na saa saba na nusu Afrika mashariki majaji hao watatangaza hadharani katika mahakama ikiwa kuna ushahidi wa kutosha kuwashtaki washukiwa hao.
Mahakama hiyo iliendesha kikao mwaka uliopita kusikiliza upande wa mashtaka na pia upande wa utetezi kutathmini ikiwa kuna ushahidi wa kutosha kuwashtaki.
Katika kesi ya kwanza, mawaziri wa zamani William Rutto , Henry Kosgey na mtangazaji wa redio Joshua Arap Sang wanatuhumiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji, kuwahamisha watu kwa nguvu, na kuwatesa watu.
Uhalifu huo unadaiwa kutekelezwa dhidi ya wafuasi wa chama cha Rais Kibaki cha Party of National Unity (PNU), katika maeneo kadhaa mkoani Rift Valley.
Kwenye kesi ya pili, Bwana Kenyatta , mkuu wa utumishi wa umma Francis Muthaura na aliyekuwa mkuu wa Polisi Hussein Ali wanakabiliwa na tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu , mkiwemo mauaji, kuwahamisha watu kwa nguvu, ubakaji na mateso.
Kiongozi wa mashtaka katika ICC Luis Moreno Ocampo anadai kwamba Kenyatta na wenzake walifadhili na kutekeleza mashambulizi dhidi ya wafuasi wa chama cha Orange Democratic Party,ODM, chake waziri mkuu Raila Odinga, katika maeneo ya Nakuru na Naivasha mkoani Rift Valley.
Watu wasiopungua 1,300 waliuwawa wakati wa ghasia hizo, na wengine zaidi ya 500,000 wakapoteza makazi.
Ghasia zilizuka baada ya Rais Kibaki kutangazwa kuwa mshindi kwenye uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali kati yake na Bwana Odinga.
Kufuatia ghasia hizo, jamii ya kimataifa iliwashinikiza Bwana Kibaki na Bwana Odinga kufanya mazungumzo ili kuzimaliza.
Mashauriano yaliyosimamiwa na katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa Koffi Annan yaliishia kwa viongozi hao wawili kukubali kuunda serikali ya mseto, huku Bwana Kibaki akihifadhi kiti cha urais, naye Bwana Odinga akawa waziri mkuu.

No comments:

Post a Comment