Thursday, December 1, 2011

. Posho za wabunge zazua mjadala- ZITTO KABWEMbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, alisema kuwa ameshtushwa na taarifa za kupandishwa kwa posho za vikao kwa wabunge huku wananchi wakiugulia ugumu wa maisha na kusema kuwa ipo siku Watanzania watawapiga mawe kwa usaliti huo.

 “Nimeshtushwa zaidi kwamba posho hizi zimeanza kulipwa katika mkutano wa Bunge uliopita kabla hata Rais hajaamua, maana maslahi yote ya wabunge huamuliwa na Rais baada ya kupokea mapendekezo ya Bunge kupitia Tume ya Bunge,” alisema Zitto.

Aliwataka wabunge wote kutambua kwamba, kuamua kujipandishia posho bila kuzingatia hali ya maisha ya mwananchi wa kawaida ni usaliti usio na mfano.

“Mbunge yeyote ambaye anabariki jambo hili labda anaishi hewani, haoni taabu za wananchi au ni mwizi tu na anaona ubunge ni kama nafasi ya kujitajirisha binafsi,” alisema Zitto.

Aliwataka pia wabunge wa Chadema, wajue uamuzi kuhusu posho ni wa chama na ni wa kisera.
“Mbunge yeyote wa Chadema anayepokea posho za vikao anakwenda kinyume na maamuzi ya sera za chama tulizoahidi wananchi wakati wa uchaguzi,” alisema Zitto.

Alisema kuwa amemwomba Katibu Mkuu wa chama chake kuitisha kikao maalumu cha Kamati Kuu ya chama kujadili suala hilo.
Alisema kuwa tangu Juni 8 mwaka huu, alikataa kupokea posho za vikao na kuwa, popote anapohudhuria vikao huwa anaomba risiti za posho anazokataa.

No comments:

Post a Comment